Msanii wa muziki kutoka nchini Tanzania, Dizasta Vina ni mmoja wa viongozi katika orodha ya wafalme wa Hip-Hop wa kizazi cha leo. Muziki wake umebeba falsafa, mafunzo na mitazamo inayogusa jamii kwa namna tofauti. Ana mtindo wa kipekee, mashairi yenye ujumbe na mtiririko wa visa na matukio ya maisha halisi ya kila siku.
Mwanzoni mwa mwaka 2021, Dizasta alitoa albamu ya "The verteller". Ni albamu yake ya pili, ina vibao 20 vinavyo ongelea tamaduni, mitazamo na imani ya vikundi mbalimbali vya watu wa jamii aliyotokea. Albamu inatoa picha ya maisha ya watu wa jamii yake, misimamo yao dhidi ya msimamo wake kuhusu masuala mbalimbali na hadithi nyingine zinazogusa nyanja mbalimbali za maisha ya binadamu.
Kabla hujaamua kwenda kununua albamu hii au kuisikiliza kwa mara nyingine fuatilia simulizi ya Dizasta Vina kuhusu safari ya kuandaa albamu ya The Verteller, hadithi za kuvutia za baadhi ya nyimbo zake, na maelezo ya kina ya ubunifu wake.
Kuhusu jina la "The Verteller".
“ Niliipa albamu jina la The Verteller kwa sababu za kisanaa na kibiashara. Jina linasikika na kuandikika kisanaa kuliko tafsiri yake kwa lugha nyingine ikiwemo lugha mama ya mwandishi, lugha ya Kiswahili. Neno 'verteller' lina maana ya ‘msimuliaji’ kutokea lugha ya Kidachi, the storyteller au rawi kwa kiingereza na kiarabu na majina mengine kwa lugha tofauti hayakuwa na mwonekano uliovutia kimaana na kiumbo kutumika kama jina la albamu kuliko 'The Verteller' na pia kwa sababu za kibiashara lilikuwa ni neno jipya kutumika kwenye kiwanda chochote cha burudani hasa kama albamu ya muziki".
Albamu inaitwa The Verteller kuwakilisha wasifu wa msimuliaji na mahala anakotoka. Jina hili linasanifu maudhui kwani albamu imesheheni masimulizi ya matukio yanayotokea mahala anapotokea msimuliaji kwa maana ya mtaa, mkoa au nchi. Dizasta Vina anasema “The verteller inaonyesha taswira ya elimu, imani, tamaduni na mila za jamii yangu na jinsi zilivyojenga mtazamo wangu wa sasa”.
Muda uliotumika kuandaa albamu.
The Verteller ilikuwa kwenye maandalizi kwa muda mrefu. Nilitumia muda mrefu kuiandaa na moja ya sababu ni kwamba kulikuwa na wazo la pili kwenye kila hatua. Mfano mmoja kwenye uchaguaji wa midundo, nyimbo nyingi zilizokuwa zimerekodiwa na midundo tofauti na ile inayosikika kwenye albamu. Muziki ulibadilishwa kila wazo jipya lilipokuja, yote ikilenga kuwa na muziki mzuri unaoendana na maudhui, hali na msisimko wa nyimbo husika. Albamu ilichukua karibia miezi 26, kuanzia kuandikwa hadi kuzalishwa na kusambazwa sokoni.
Wimbo unaomuhusu yeye binafsi.
“Kuna nyimbo nyingi ambazo zinanihusu mimi, karibu zote japo sio kama hadithi zinavyosema lakini falsafa nyuma ya hadithi au mitazamo ninayowakilisha. Kuna nyimbo zinanihusu moja kwa moja, mfano 'Yule Yule' - Yule yule nimezungumzia mahara nilipotoka, jinsi nilivyoishi, watu na itikadi zao, jinsi wanavyo ishi huko, na jinsi wanavyoona jamii ya watu wengine. Nyimbo nyingine zote ni simulizi za kubuni lakini zinaendana na hadithi ambazo nimezitoa mtaani kwangu”.
The verteller ni wasifu wa maisha ya mwandishi ambaye ni mimi. Naonyesha nilipotoka kukoje, kwa mfano hadithi za “Kibabu na binti” zipo kwenye mitaa niliyotoka, “Tattoo ya asili” zipo kwenye mitaa niliyotoka, “Confession of a mad man” ambayo inaonyesha jamaa anakutana na binti anamwambia binti ondoka, usipoondoka nitakufanyia hiki na kile binti anahisi anamtania, ni sitiari ya watu wanaotoka kijijini na kuingia mjini kwa mara ya kwanza. Kuna kuwa na kila dalili mbaya ya kupata shida akija mjini lakini anapuuzia dalili hizo kwa matumaini kwamba labda siku moja mambo yatakuwa bora zaidi. Zote hizi zina wakilisha baadhi ya maadili na falsafa ninazoziamini, kwahiyo zinanihusu kwa njia moja au nyingine.
Utofauti wa albamu ya ‘The Verteller’.
Utofauti wa albamu ya “The Verteller” na album nyingine nyingi za Hip Hop hapa Tanzania ni kwamba ni wasifu wa msimuliaji na mahala alipotoka (Biography). Msimuliaji anaeleza jinsi mwanamke anavyoonekana, na nafasi yake katika jamii, masuala ya mahusiano jinsia na watoto, uhuru wa kuongea na vyombo vya habari, ukimwi na watoto wa mitaani, usalama na mtoto anavyoonekana kwenye jamii yake na vile anavyolelewa. Msimuliaji anaeleza hivyo vitu vilivyo athiri namna anafikiria na vile anavyoishi. Ni miongoni mwa albamu chache ambazo zimefanywa hivyo.
Kwa mtazamo wa kisanaa ni albamu ambayo asilimia 90 ya nyimbo ni hadithi ambazo visa vyake zimebuniwa lakini zinaelezea mambo yanayohusiana na sehemu msimuliaji ametoka. Ni albamu ya simulizi, kitu ambacho hakijawahi kutokea Tanzania lakini pia ni wasifu wa msimuliaji, inaonyesha msimuliaji tangu anaanza alipozaliwa mpaka hapa alipo, kule alikotoka na jinsi jamii ilivyomlea, mabaya na mazuri aliyoyaona kwenye jamii yake ndio anakuja kuyasimulia.
Wimbo uliochukua muda mrefu kuuandaa.
Kuna nyimbo kadhaa zilichukua muda mrefu, Hatia namba nne ni mojawapo kwa sababu ilibadilishwa kutoka kwenye riwaya kuwa wimbo. Anasema “ilitakiwa nipunguze baadhi ya vitu nijue kitu gani ni muhimu sana kukiweka kwenye wimbo, kitu gani nikitoa kitaharibu maana na mtiririko wa sehemu za wimbo au wimbo mzima”.
Ilichukua muda mrefu kurekebisha kwa sababu kulikuwa na mabadiliko mengi - inatakiwa utengeneze wimbo, utengeneze namna utawakaribisha wasikilizaji kwenye wimbo, uwashawishi wabakie halafu uwapeleke kwenye uelekeo mmoja baadae ubadilishe ule uelekeo haraka kuleta mvuto kwenye hadithi. Ili kuwa ni kazi ngumu kuiandaa, hata Ringle Beats ilimchukua muda mrefu kwa sababu tulijaribu midundo mingi na kubadilisha maana mingine ilikuwa inaharibu hisia za wimbo, mwisho wa siku tulipata mdundo sahihi, tukaufanyia kazi na watu wakaupenda.
Kuhusu kutayarisha muziki na Ringle Beats.
Mimi na Ringle Beats tumekuwa marafiki kwa miaka mingi sana, tumefahamiana mwanzoni mwa mwaka 2011 ni kama miaka 10 sasa na tumekuwa marafiki tangu hapo. Alitayarisha nyimbo ya kwanza ya Panorama ya mimi na Dubo na kutoka hapo tumekuwa karibu. Ametayarisha nyimbo zangu nyingi, Kanisa, Siku mbaya, NIS3, Waite hakika tumekuwa marafiki kwa muda mrefu. Alikuwa mtu wa kwanza kumfikiria lilipofikia wazo la kusema nifanye na mtayarishaji gani.
Ringle Beats alikuwa mtu wa kwanza kumfikiria kwa sababu tunafahamiana muda mrefu na nafahamu uwezo wake wa kutayarisha kazi, pia ana historia ya kufanya shughuli za muziki kanisani kwenye kwaya, ana utaalam na mbinu nyingi za kutayarisha na kuchanganya muziki. Ni mhandisi mzuri wa sauti, pia ni mbunifu anapiga kinanda vizuri, gitaa na ala nyingine za muziki, ana uwezo mkubwa kwenye kutayarisha muziki. Tumefanya na watayarishaji wengine kadhaa ambao walikuja kuchangia utaalam na maoni yao. Cjamoker na Jcob walichangia "mixing na mastering" na kuna watayarishaji wengine lakini mtayarishaji mkuu ni Ringle Beats. Kwenye kuandaa muziki uwezo wake unagusa sehemu kubwa ya utayarishaji hii ilikuwa ni faida sana kwangu.
Wimbo maalum zaidi.
Nadhani albamu nzima ni maalum kwangu, lakini kuna nyimbo ambazo naona kwangu ni maalum zaidi. Hatia namba nne ni maalum sana kwangu kwa sababu nilitaka kuandika kitabu lakini nikaona inafaa sana kuwa wimbo, nilirekebisha vitu vingi ili kitabu kiwe wimbo, utayarishaji wake ulisumbua kubadilisha mawazo kutoka kwenye kitabu kuwa wimbo, hakika kila wakati nikisikiliza huu wimbo najisikia fahari sana kwa jinsi ulivyotoka.
Lakini Mwanajua ina maana binafsi kwangu, maana ambayo nimeacha watu waitafute. Kuna watu ambao tayari wanajua maana ya Mwanajua kwa sababu wameelewa fumbo nililoliweka kwenye wimbo. Watu wengine wametengeneza maana zao jambo ambalo ni sahihi kwa sababu sijawahi kuiweka hadharani kila mtu akaelewa maana yake, kuna watu wanaohisi ni binti mrembo, wengine wanahisi ni umaarufu ambao unakuja na kuondoka, vyeo, maisha yanakuja na kuondoka wote wapo sahihi nilichotaka ni wimbo kugusa watu, kama wimbo umekugusa na umetengeneza maana yako binafsi ni sawa, kwa hiyo mwanajua ni maalum kwangu, yule yule ni maalum zaidi kwangu kwa sababu unahusu msimuliaji mwenyewe.
Ujumbe uliojificha kwenye mpangilio wa nyimbo.
Mpangilio wa jumla wa albamu ni kwamba msimuliaji anazaliwa, msimuliaji anajifunza na kisha anafanya makosa, anaingia kwenye mapenzi, anajuta, msimuliaji anapata faraja na mwisho wa siku msimuliaji anakufa. Maudhui kadhaa ya mwanzo yanaonyesha kuanza yani mwanzo, maudhui yanayofuata yanaonyesha kukua, maudhui ya katikati yanaonyesha makosa na maudhui ya mwisho yanaonyesha msimuliaji anakufa. Mpangilio wa jumla hakuna nyimbo maalum zinazoeleza kuzaliwa na kufa lakini maudhui yaliyopo kwenye maeneo ya mwanzo, katikati na mwisho yanaonyesha yupo kwenye kuzaliwa, kukua, kufanya makosa, kutubu na kisha kufa.
Msukumo katika kuandaa albamu.
Dizasta anasema “nilisikiliza sana albamu ya ‘Mi Mmasai’ ya Mr Ebo na ‘Machozi, jasho na damu’ ya Professor Jay wakati naandaa albamu hii kwa sababu hizi albamu zilikuwa na maudhui mengi sana. Nilikuwa nafuata msukumo chanya humu, lakini nilikuwa nanoa ufundi wa kutiririka kutoka kwenye sanaa nyingine tofauti ila katika kuandaa The Verteller nilipata msukumo zaidi kwenye hizi kazi mbili”.
Maudhui ya albamu.
Dhamira kuu ya albamu ni uhuru wa kuzungumza na kujieleza ndio maana utangulizi unasema msimuliaji aachwe huru ili waovu watangazwe na wema washangiliwe. Kuna dhamira nyingine ndogo ndogo nje ya wazo kuu nazo ni kama ifuatavyo.
Dizasta Vina anamzungumzia mwanamke anavyoonekana kwenye jamii yake ambapo wengi wanamtumia kama chombo cha starehe, wengine wanaona kama hana sauti hivyo mawazo yake hayaheshimiki kwenye jamii ambayo msimuliaji katoka (binti anabakwa kwenye wimbo wa tatuu ya asili). Kwenye albamu hii mwanamke pia anazungumziwa kama kiongozi kwenye jamii yake, wimbo wa "A confession of a mad son" na sehemu kadhaa za wimbo wa "Yule yule" msimuliaji anaeleza alivyolelewa na mama yake, hii inaonyesha nafasi ya mwanamke kama kiongozi.
Msimuliaji pia anazumgumzia masuala ya jinsia na nafasi za kila jinsia kwenye jamii, wimbo wa "Mascular feminist" na sehemu baadhi za "Wimbo usio bora" zinazungumzia nafasi ya kila jinsia kwenye jamii.
Masuala ya maadili yamezungumziwa kwenye nyimbo kama "Wimbo usio bora" na “Mlemavu” ambapo mume ana mlalamikia mwanamke kubadilika na kukosa maadili, pia kwenye "Tatuu ya asili" vijana walimbaka binti kwa kukosa malezi mazuri yaliyopelekea kuwepo kwa mmomonyoko wa maadili.
Kwenye nyimbo kama "Ndoano" na “wimbo usio bora” amezungumzia mapenzi, mahusiano na ndoa, nyimbo nyingine zilizogusa masuala ya mapenzi ni pamoja na “Mlemavu”.
Pia kwenye wimbo wa "A confession of a mad philosopher" na wimbo wa "Kifo" msimuliaji amezungumzia falsafa nyuma ya pumbazo la uhuru wa nafsi na hiari ya kufanya maamuzi (Free will illusion).
Dhamira nyingine ndogo ndogo zilizoonekana kwenye huu mradi ni kama uhuru wa vyombo vya habari, watoto wa mtaani, ukimwi, umuhimu wa elimu kwa jamii na matumizi mabaya ya madaraka, wimbo wa "Tattoo ya asili" mwalimu alikatazwa kuongea na kiongozi, alitumia nafasi yake kukandamiza maoni ya watu wengine na pia alizongwa na ujinga. Dizasta Vina anasema "Sehemu ambayo elimu itadharauliwa na kuwekwa chini ndio sehemu ambayo matatizo yataibuka" kwa hiyo kuna umuhimu wa elimu kwa jamii.
Dizasta amejadili madhara ya mihadarati, kamali na Rushwa kwenye wimbo wa “Money”, ukimwi na tabia chochezi kwenye kuenea kwenye “tatuu ya asili” na athari za kuwepo kwa watoto wa mitaani.
Kuna mgogoro kati ya kundi na kundi au mtu na mtu. Mfano, wanandoa wana kwazana kwenye “Wimbo usio bora”, kiongozi na wananchi kwenye “Tatuu ya asili”, askari na raia kwenye “Money” na baba na mtoto kwenye “Kibabu na binti”.
Pia kuna migogoro nafsi au dhahania. Mfano, mwandishi anaongea na kifo nafsini kwenye wimbo wa “Kifo”, anawaza kuhusu uhuru wa nafsi kwenye “Confession of a mad philosopher”, mwanamke na mwanaume “muscular feminist”, pia mwandishi anawaza jinsi Mwanajua alivyoondoka baada ya kutamba sana “Mwanajua”.
Mwandishi amejadili matatizo ya afya ya akili alipojadili ugonjwa unaoitwa “ASPERGERS” ambayo ni hali inayosababisha kukosa uwezo mzuri wa kuchangamana na jamii na kuwasiliana. Kwenye wimbo wa “Yule yule” Dizasta alikili kuwa na hali hiyo.
Dizasta anatupa jumbe kadhaa. Mfano, anasema umaarufu, pesa na vyeo vinapita kwenye “Mwanajua” na “Almasi”, elimu ni ukombozi kwenye “Tatuu ya asili”, tamaa inaponza kwenye “Money”, ndoa si mafanikio kwenye “Ndoano”, usawa ni fursa si matokeo kwenye “Muscular feminist” na uhuru si kitu halisi “Confession of mad philosopher ”.
Nunua albamu hii au isikilize kwenye Audiomack, Boomplay na mitandao mingine na tufahamishe nyimbo unazozipenda kwenye albamu kupitia kurasa za Panorama Authentik kwenye Facebook, Instagram na Twitter.
Mwaka 2024 unaelekea ukingoni, Kwa hitaji la wengi nimeandaa list yenye baadhi ya Albums nilizosikiliza, vitabu nilivyosoma, makala nilizosoma na filamu nilizoangalia kwa mwaka huu wote.
VITABU
Mwaka huu nilisoma vitabu vitatu na hii ndio review yangu kwa ufupi kwa kila kimoja.
1. Ujamaa - Essay on Socialism - The late Julius K. Nyerere
Kitabu kilichapichwa kwa mara ya kwanza mwaka 1961, na kufanyiwa marejeo mara kadhaa na baadaye kutafsiriwa kwa lugha ya kiingereza mwaka 1968. Nilikisoma kwa mara ya kwanza mwaka 2013 lakini nikawiwa kurudia sasa nikiamini kuwa na uwezo wa kuelewa maudhui yake kwa mapana yake. Kwenye nakala hii mwandishi anajadili maono ya hayati Baba wa taifa Julius Kambarage Nyerere kuhusu wazo lake la kuwepo kwa aina maalumu ya ujamaa inayoendana kwa asilimia mia moja na tamaduni, mira na desturi, aina ya itikadi, kiwango cha uelimikaji na mtindo wa maisha wa nchi za kiafirka (Specifically Tanzania). Wazo la aina hii ya ujamaa lilitumika kama sera kuu ya chama cha siasa cha TANU ambacho Mwalimu alikuwa ni mwenyekiti wake. Mwandishi alielezea mafanikio na changamoto ya wazo hili hasa kwenye practicability and implimitations. Nakala hii ilibaki kumbukumbu ya juhudi za mwanzo za kumkomboa mwananchi masikini baada ya Ukoloni. Hili andiko lilisanifisha kanuni muhimu zilizosimamia haki na usawa kama zilivyojadiliwa kwenye azimio la Arusha. Nukuu yangu pendwa kutoka kwenye nakala hii ni ile iliyomnukuu mwalimu kuhusu umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii kwa ustawi wa familia zetu, akisema "‘Mgeni siku mbili;
siku ya tatu mpe jembe’
2. The moral Lanscape - How science can determine human values - Sam Harris
Binadamu wa karne ya 21 wamekuwa kama kitu kimoja kwa sababu ya kukua kwa teknolojia hasa kwenye eneo la mawasiliano na usafirishaji. kukua huku kumefanya dunia kuwa ndogo. Binadamu wanajijamiisha kwa karibu na kwa haraka zaidi bila kujali maeneo waliopo. Hii imekuza umuhimu wa mazungumzo kuhusu falsafa ya maadili. Mwandishi wa The Moral Landscape, Kitabu kilichochapishwa mwaka 2010, Sam Harris anajadili wazo la kuhusianisha maadili na ustawi wa maisha ya binadamu (Well-being) akisema Mijadala ya maadili haitakuwa na maana kama haitahusisha ustawi wa maisha ya binadamu na wanyama. Pia alijadili kwa kiasi gani sayansi itaweza kutupa kweli ya nini maana ya ustawi hasa kwenye eneo la afya ya akili, mwili na hisia za binadamu. Pia alijadili tamaduni na imani mbalimbali zinavyoweza kuhatarisha afya ya mwili, akili na hisia, lakini pia afya ya uchumi wa binadamu. Nukuu yangu pendwa kutoka kwenye kitabu hiki ni "Wanawake na wanaume walio kwenye hukumu za kunyongwa, wapo pale kwa sababu ya mchanganyiko wa malezi mabaya, mawazo na itikadi mbaya, imani mbaya, vinasaba mbaya au bahati mbaya"
3. Who we wrestle with God - Jordan Peterson
Kitabu hiki kilichapishwa November 2024, Ndio kilikuwa kitabu cha mwisho kusoma mwaka huu. Mwandishi anajadili hadithi za mwanzo kabisa za kifasihi na umuhimu wake kwenye maisha ya sasa. Mwandishi anaamini kuwa fasihi za zamani ni muhimu kwa sababu zinatupa picha ya mtindo wa kufikiri wa jamii za kale (their thinking process). Mwandishi pia anajadili dhana ya ukaidi, sadaka, mateso na ushindi kwa kutumia hadithi mbalimbali za kibiblia. Jordan anachagua Biblia kuelezea subject matters zake akiamini ni kitabu stahiki zaidi kiushawishi, kiumri na kiuhalisia (authenticity). Moja ya subject matter alizojadili mwandishi ni IMANI na kujitoa SADAKA (Faith and sacrifice). Anasema dunia na mapana ni kubwa sana kiasi hatuwezi kuimaliza kuielewa hivyo kwenye maisha mafupi ya binadamu huwa tunachagua vile tunaavyoona ni muhimu. Na hapo ndio Imani na sadaka vinapokuja kwani kuchagua ni kuamini kuwa upo sawa na machaguo yako na unatoa sadaka vingine vyote ili kufuata unachoona ni sahihi (cost of choices/opportunity). Mfano wa hadithi alizotumia kujadili maudhui ni ile hadithi ya Yona aliyeikimbia sauti ya Mungu iliyomtuma kwenda Nineveh kueneza habari njema, Yona alikaidi na mwishowe kumezwa na samaki. Mwandishi alihusisha hii hadithi na athari za kukimbia majukumu kwa nafasi uliyopewa. Nukuu yangu pendwa kwenye kitabu hiki ni "kanuni mbaya zikienziwa, wafalme wabaya wakisimamishwa na maadili mabaya yakiwekwa na watu, ni watu wenyewe ndio wataangamia"
FILAMU
Nilipata wasaa wa kuangalia filamu kadhaa mwaka 2024 na hizi ni 5 zilizonivutia zaidi.
1. 12 angry men ya mwaka 1957
Filamu inahusu baraza la waamuzi 12 waliopewa jukumu na mamlaka ya kuamua kesi ya kijana aliyetuhumiwa kumuua mzazi wake. Kesi iliyoonekana ni ya dakika kadhaa tu kwa sababu ya nguvu ya ushahidi uliowekwa ila inageuka kuwa shughuli ya kichunguzi. Waamuzi 11 waliamini kuwa mtuhumiwa ni mkosefu na anastahili adhabu wakati mmoja akiwa na shaka na aina ya ushahidi ulioletwa, hivyo akachukua jukumu kuwashawishi waamuzi wenzake kujadili upya ushahidi ili kuondoa shaka. Filamu ya seti moja ila ilikuwa na uwezo wa kubakisha shauku muda wote kwa sababu ya ubora wa mazungumzo na story progression. Moja ya nukuu niliyoipenda kwenye Filamu hii ni "Kama unataka kupiga kura kuwa fulani ana hatia, sema kwa sababu una uhakika ana hatia na sio kwa sababu umechoka kusikiliza shauri". Mtoa nukuu alikuwa anajaribu kuwaambia waamuzi wengine kuwa wasitoe maamuzi wa sababu wamechoka na wanataka kwenda nyumbani
2. Schindller's list -1993
Filamu ya wasifu wa kweli (Autobiography) inayomuhusu Oskar Schindler, Mfanyabiashara mwenye tamaa ya pesa aliyeingiwa na ubinadamu kiasi kugeuza kiwanda chake kuwa kimbilio la wayahudi waliothiriwa na serikali ya ki-nazi ya Ujerumani. Filamu hii iliandaliwa kuenzi mchango wa Oskar kwenye mapambano dhidi ya ukatili wa serikali ile chini ya Adolf Hitler. Moja ya nukuu muhimu niliyoipenda kwenye Filamu hii ni "Nguvu ni pale ukiwa na kila sababu ya kuua alafu hauui" akijadili umuhimu wa kusamehe na moja ya wafanyakazi wa serikali ya kibazazi ya ujerumani.
3. Enemy - 2013
Filamu ya kisaikolojia inayomuhusu mhadhiri wa chuo kikuu anayemuona mtu anayefanana naye kwa asilimia 100 kwa mara ya kwanza baada ya kuambiwa na rafiki yake kuwa wamefanana. Anaenda kuangalia filamu zake baada ya kugundua ni mwigizaji. Kiu ya kumchunguza inaishia kumuweka kwenye njiapanda inayozaa matatizo makubwa. Mhadhiri huyu analea mazoea yake ya kuchunguza familia ya mtu huyu na mwishowe kuingia matatani. Filamu inayojadili umuhimu wa kurekebisha mazoea mabaya kabla hayajawa tabia. Mazoea kwenye filamu yanawakilishwa na buibui mdogo anayeonyeshwa mwanzo wa filamu kisha kuwa mkubwa mwisho wa filamu.
4. The Assasionation of JESSE JAMES by the Coward ROBERT FORD - 2007
Mja mwoga Robert Ford anategemea kulakiwa kishujaa na jamii yake baada ya kumuua jambazi anayeogopwa kwenye mji wake. Kiu ya umaarufu na heshima inamfanya kubadili jina kisha kuandika kitabu kusheherekea mauaji yake mwenyewe lakini bado jambazi Jesse anaimbwa kama shujaa huku yeye akiwa hatambuliki kabisa. Hasira inampanda baada ya filamu kutengenezwa kumuenzi Jesse. Robert anajaribu kuishi na uhalisia kuwa watu hawamwoni kama shujaa bila mafanikio, Kiu yake ya kuheshimiwa inarudi na mwishowe inamwingiza kwenye kifo.
5. Cosmos: A Spacetime Odyssey, Season 1
Msimu wa kwanza wa mfululizo wa sukununu ya binadamu kuhusu ulimwengu na elimu ya anga. Chaneli ya National Geographic wanaungana na Mkufunzi wa masuala ya astrofizikia Neil de Grease Tyson kubadili kitabu kuwa onyesho la televisheni.
ALBUMS
Nilisikiza album kadhaa kwa minajiri ya burudani na elimu na hizi ndio zilinivutia zaidi.
Waraka huu utumike kama mashitaka kwa binadamu kwa kushindwa kuishi kwenye daraja la ustaarabu wake, Ustaarabu anaokwezwa kuwa nao. Utumike kama mashitaka kwa kushindwa kuwajibika na kutumia vyema vipawa alivyozawadiwa na asili. Namtuhumu binadamu kwa kuwa kiumbe mbaya sio tu kwa wanyama wengine na mazingira, bali hata kwa binadamu wenzake. Namtuhumu kwa kuwa MJIVUNI, MNAFIKI, MCHOYO, MWONEVU, MUUAJI, MWONGO, MKATILI, MJINGA, MSHENZI na MBINAFSI na nipo tayari kusimamia tuhuma hizi kwa niaba ya wanyama wengine wafugwao na wasiofugwa. Kwa kuanza, nina maswali makuu kwake.
Amestaarabika?
Nina shaka na maana na kipimo cha ustaarabu kwa sababu kuu mbili.
- Moja, uhalisia hauonyeshi hivyo, ni ngumu kujadili ustaarabu na kiumbe ambaye amemiliki na kuuza binadamu mwenzake kama bidhaa kitumwa, ametoa sadaka ya damu, amepigana vita kadhaa akigombea miliki ya ardhi, mipaka na rasilimali ambazo akifa anaziacha, anabagua haki ya umiliki wa rasilimali kwa kigezo cha jinsia na rangi, ukabila au utaifa na pia ngumu kujadili ustaarabu na kiumbe anayefuga majeshi kujilinda dhidi ya binadamu wenzake. Hizi na nyingine nyingi si dalili za kustaarabika.
Pili, vyote (maana na kipimo cha ustaarabu) vimewekwa na yeye binadamu, kumjadili binadamu bila muktadha linganishi nje ya jamii yake. Labda ndiyo maana ustaarabu unapimwa kwenye kutendea usawa kwa binadamu tu na si viumbe wengine na mazingira (UBINAFSI). Kifupi kwenye mtihani, mtunzi ni binadamu, mfanyaji ni binadamu na msahihishaji ni yeye mwenyewe.
Tukikubali binadamu kastaarabika, viumbe wengine wanafaidikaje na kustaarabika kwake? Asili imemjaalia binadamu nguvu kuu tano.
Ufahamu: Uwezo wa kupokea na kutafsiri taarifa kwa muktadha na maana sahihi kiasi kuweza kufanya mrejesho stahiki.
Mantiki: Uwezo wa kupangilia mawazo kwa uyakinifu wa kimaana na kimuktadha.
Kutambua kuwa anaishi na kurindima na maisha, na kuhisi thamani ya uhai (being sentient).
Lugha: Chombo cha kimapinduzi kinachomuwezesha kusafirisha taarifa haraka na kwa ufanisi wa hali ya juu).
Hivi vipawa ni muhimu. Kwanini ni muhimu pia kwa viumbe wengine? Binadamu ni Kiumbe wa kijamii (a social being), ana majukumu ya kijamii (kwa viumbe na mazingira). Kuyafunga majukumu hayo kwa binadamu pekee ni UCHOYO. Wanazuoni walisema, palipo na nguvu kubwa, pana jukumu kubwa, (where there is great power, comes great responsibility). Ni muhimu kuhakikisha anashirikisha viumbe wengine mafanikio ya karama hizi na si kuwasababishia changamto tu.
Kumiliki mnyama kunakinzana na dhana ya kustaarabika?
Miaka na miaka binadamu amemiliki mnyama kwa chakula, ulinzi, urembo, mavazi n.k, kama kumiliki mnyama kwa ajili ya mavazi na urembo si haja kuu ya asili ya maisha kwa binadamu.
Je, binadamu aliumbwa kula nyama kiasili ? na tunamtambuaje mnyama mla nyama kiasili?
Tuchunguze jedwali:
SIMBA
BINADAMU
Ana kasi ya kukimbiza windo
Hana kasi ya kukimbiza windo anatumia mitego, silaha na kulaghai (kufuga)
Ana kucha za kurarua
Hana kucha za kurarua, anatumia nyenzo mfano kisu
Ana machonge ya kuchana
Hana machonge ya kuchana, anatumia nyenzo
Ana mataya yenye nguvu ya kutafuna nyama
Hana mataya yenye nguvu ya kutafuna, anaunguza na moto na mafuta/maji kwanza
Mfumo wake wa kumeng'enya unaweza kumeng'enya nyama
Mfumo wake wa umeng'enyaji hauwezi kumeng'enya nyama mpaka iunguzwe
Nyama ni chakula kikuu, hana mbadala wa chakula zaidi ya nyama
Nyama si chakula kikuu ni ziada
Anawinda kwa ajili ya haja ya asili ambayo chakula tu
Anafuga kwa ajili ya haja za ziada kama ladha ya muda mfupi, na kuzalishia bidhaa kama mavazi na mikoba
Utagundua kuwa binadamu aliundwa na asili kuwa mwokota matunda, mchimba mizizi, mbegu na mboga mboga. Mikono yake, kucha zake, meno na mfumo wake wa uvunjaji chakula vyote vinaonyesha binadamu ni Herbivore.
UTUMWA NA UFUGAJI
Utumwa ni pale ambapo binadamu mmoja anammliki binadamu mwingine kama bidhaa au mali kwa ajili ya matakwa binafsi kama uzalishaji na usaidizi BILA RIDHAA YA ANAYEMILIKIWA na pia bila malipo au marejesho (consideration/remuneration).
Ufugaji ni pale ambapo binadamu anammiliki mnyama kwa ajili ya chakula, usaidizi na sababu nyingine binafsi.
Kuna mstari mwembamba sana kati ya maana ya utumwa na ufugaji.
Umiliki wa kiumbe mwenye nafsi, damu, nyama na mifupa na ufahamu bila idhini yake wala makubaliano kwa sababu binafsi haitofautiani sana kimaana na utumwa kama ambavyo kuchinja kwa ajili ya chakula hakutofautiani na UUAJI.
Tuchunguze jedwali la 2:
UTUMWA
UFUGAJI
Binadamu ni bidhaa/mali/kizalisha mali
Mnyama ni bidhaa/mali/kizalisha mali
Binadamu ananunulika/kuuzika kubadili umiliki (transfer of ownership)
Mnyama ananulika/kuuzika kubadili umiliki
Hakuna thamani ya ndani ya mtumwa bali ile inayopimwa na nguvu yake ya uzalishaji/utimizaji wa haja ya mmiliki (no intrinsic value). Mfano: Binadamu ni bora akiwa anazalisha bidhaa, mrembo kumvutia mmiliki n.k
Hakuna thamani ya ndani bali ile inayopimwa na nguvu ya uzalishaji/utumizaji wa haja ya mmiliki (no intrinsic value). MFANO Ngómbe ni mzuri akiwa anazaa au kuzalisha, anatoa maziwa kwa ajili ya mfugaji n.k
Hakuna marejesho/malipo kwa anayemilikiwa
Hakuna marejesho/malipo kwa anayemilikiwa
Miaka bora ya anayemilikiwa (akiwa na nguvu na afya) ni miaka ya kumtumikia mmiliki Mf. binadamu mwenye nguvu, kijana, mrembo , mwenye kasi anamtolea hizi zawadi zote mmiliki na si kwa ajili yake
Miaka bora ya mnyama (akiwa na nguvu na afya) ni miaka ya kumtumikia mmiliki. mf. Ng'ombe akiwa na maziwa mengi si kwa ajili ya ndama wake bali ni kwa ajili ya mfugaji, akiwa na afya ni kwa ajili ya chakula cha mmiliki na si kwa ajili ya maisha yake
Licha ya mfanano huo, kimoja ni halali na kingine ni haramu kisheria. Hapo unagundua legality is not about morality. Kwanini hizi tuhuma ni valid kumwelekea binadamu, hasa ikiwa wapo viumbe wengine wanakula wanyama wenzao? Kwa kiumbe anayenadi ufahamu, mantiki na kustaarabika ni mashitaka stahiki kabisa.
Mimea nayo ni viumbe?
Mimea ni viumbe lakini wamekosa kitu kimoja muhimu, Sentience, uwezo wa kujua iko hai na kuwa na vitambuzi vya hali tofauti uhai (furaha na huzuni, hasira, wivu, kero baada ya bugdha, upendo, huruma, tamaa au hamu ya ngono) (si maelezo rasmi ila maana sahihi). At least haijathibitika kuwa mmea una huu utambuzi hasa kwakuwa unahitaji ubongo au mfananao wa ubongo kiufanyaji kazi kutafsiri hisia hizi. Labda ndio maana ni bora kuanza kula mimea kabla ya wanyama wenzio. Kama ambavyo hawezi kumla binadamu mwenzake palipo na ngombe, ndivyo ambavyo hawezi kumla ngombe palipo na matunda. Inaitwa kupima degree of necessity. Asili haijaonyesha binadamu hatakiwi kula viumbe, La hasha imeonyesha hatakiwi kula wanyama.
WAZO: ukiwa kwenye mtumbwi uliopotea baharini, yapo matunda, nyani mmoja, mbuzi mmoja na mtoto mdogo. Ukiwa kwenye hali ya kawaida kiakili utaanza kula matunda kisha mbuzi, kisha nyani alafu inapobidi kutimiza golden rule kuwa hakuna bora zaidi ya uhai wako utamla binadamu kwa mapambano. Nje ya hii order ni shaka la ufahamu.
Ipo nafasi sawa ya kupigania uhai kwa viumbe walao nyama?
Kiasili, kila kiumbe mla nyama ameundwa na nafasi sawa ya kupigania maisha. Ndio maana simba anaingia mawindoni kupambana na swala ambaye naye asili ilimuunda kujua na kukimbia hatari. Simba atapambana na atapata chakula kimoja kwa wakati mmoja, inaitwa fair chance to fight for survival na ipo kwa ALL SENTIENT BEINGS. hii ni sawa kwa chui, duma, mamba n.k isipokuwa binadamu. Binadamu ana njia zisizo za asili kupata chakula kwa sababu sio chakula chake cha asili. moja ya sadaka anazotoa ni kutotoa nafasi sawa kwa viumbe wahanga kupigania maisha yao akiamua kuwafuga, kuwategea mitego au gesi za sumu si nafasi sawa ya kupigania uhai. Kama binadamu ana akili ya kuunda vifaa haimaanishi ana uhuru wa kutumia vifaa hivyo kuumiza. MWONEVU.
WAZO 2: Maluweluwe ni kusema virutubisho muhimu vinapatikana kwenye wanyama tu. Ni binadamu tu anashinda kwenye viwanja vya mazoezi kupunguza mwili, ni binadamu tu anasumbuka na Obesity (unene kupita kawaida) na ni binadamu tu anayeumwa magonjwa ya moyo. Kiasilia kundi la primates wote ni wala mimea, kama Orangutani, Bonobo, chimpanzii n.k ni wanyama wa karibu na binadamu kibaiolojia, kifiziolojia na kianatomia, binadamu hawezi kusimama nao hata kidogo kwa nguvu, kasi au ustahimilivu dhidi ya kiu, njaa na maradhi na ni wala mimea. Labda tuwaulize mamalia wakubwa zaidi mwituni Tembo na Kifaru wanapata wapi virutubisho ikiwa wao pia ni wala mimea? Virutubisho ni sababu ya UONGO.
Mungu kaumba wanyama kuliwa na binadamu?
Mungu (anayeshuhudiwa na binadamu) aliumba wanyama waliwao kama chakula akawapa milango ya fahamu, neva za maumivu, hofu na haja kuu ya kuishi. Rudia hiyo sentensi iliyopita tena. Mnyama anapochinjwa anasikia maumivu kwakuwa ameumbiwa vihisi maumivu, anasikia dhuruma kwakuwa ameumbiwa haja ya kuishi na anasikia hofu kwakuwa pia ameumbiwa wasiwasi. Mungu wa huruma na upendo kwa binadamu tu, alishusha kitabu cha uongozi kwa binadamu tu kuruhusu matumizi ya wanyama kama chakula. Kinachosikitisha zaidi ni kwamba, hizi ni busara za vitabu vinavyosemwa ni vitakatifu na vina elimu na busara zisizo na kipimo.
WAZO 3: Basi nami nakuja na Kitabu cha Mungu wangu, Mungu wa wanyama, Mungu anaitwa ASILI, dini inaitwa MANTIKI na dhambi pekee ni kuwa MJINGA.
Ni Mungu yupi ambaye hajajua daraja la juu zaidi la ustaarabu,upendo na huruma?
Kupenda, kuheshimu na kulinda binadamu ni daraja la ustaarabu, Kupenda, kuheshimu na kulinda wanyama ni daraja la juu zaidi la kustaarabika. Binadamu wastaarabu hawajajua daraja hili, Lakini cha ajabu ni kwamba hata nguvu kuu ya imani zao (MUNGU) naye hajajua daraja hili la juu la kustaarabika. Kama ambavyo tumesubiri miaka na miaka Utumwa na biashara yake kutangazwa ni haramu, basi tusubiri miaka mingine mingi biashara ya kitumwa ya wanyama iwe haramu. AU TUSUBIRI MPAKA SIKU WANYAMA WAONGEE KUWA WANAONEWA NDIO TUAMINI?
WAZO 4: Unahitaii Mungu kusema jambo ni baya ili liwe baya? Na je, jambo ni baya kwa sababu mungu kasema au ni baya ndiyo maana mungu kasema?
Binadamu ni wa maalumu kuliko viumbe wengine?
Kujua umuhimu na umaalumu wa kitu ni kupima changamoto kipindi hakipo. Hii ni mifano ya kimantiki ya yatayotokea ikiwa binadamu atatoweka. Joto litapungua kwa sababu hewa ya kabonidioksaidi itapungua. Hewa hii inazuia joto kuondoka duniani. Binadamu anazalisha zaidi hewa hii kwa kuunguza ghafi za kaboni na visukuku(fossils) kwa shughuli mbalimbali binafsi, Ozoni itafunga kabisa kwa sababu inapata mushkeli kwa uzalishaji wa hewa chafu unaotokana na shughuli za kibinadamu, Uzalishaji wa chupa za plastiki utaisha, kelele za viwanda na vyombo moto zitaisha, Uharibifu wa mazingira kwa sababu ya vita na shughuli nyingine kama uchimbaji madini, kilimo na ujenzi utaisha. Udongo utasheheni rutuba, kifupi dunia itapona vidonda.
Umuhimu wa binadamu upo wapi? Ikiwa Phytoplanktoni inazalisha karibia asilimia 70 ya oksijeni duniani, Nyuki ambao ni wachavushaji wa karibia theluthi moja ya mimea inayomea ardhini kwa njia hiyo kuzuia dunia nzima kuwa jangwa? Minyoo midogo ya udongoni wanaendesha mzunguko wa rutuba udongoni? viumbe ambao wakiondoka sio tu binadamu atakufa bali hata dunia itatikisika.
Umaalumu wa binadamu upo wapi? ikiwa ameundwa na vijenzi vile vile vilivyounda sehemu kubwa kama si yote ya ulimwengu, Haidrojeni, Oksijeni,kaboni na Naitrojeni. Namtuhumu binadamu UJIVUNI wakati vipo asivyoviweza, asivyovijua na vipo muhimu na maalumu zaidi yake.
Kama ni maalumu kwa sababu ya uwezo wa kuongea, kuwasiliana, kujenga n.k basi tai ni maalumu kwa sababu anaona mbali, kinyonga ni maalumu kwa sababu anaweza kunakiri rangi za mazingira akinuia kujificha, popo ni muhimu analala akining'inia kichwa chini miguu juu, ndege anapaa, samaki wanapumua kwenye maji. Umaalumu unapotea ikiwa kila mtu ana kipawa chake.
Je kufuga na kula ni vyema kwa sababu imehalalishwa kisheria?
Being legal, does not mean moral all the time. Kitu kuwa halali haimaanishi ni adilifu. Miaka kadhaa nyuma utumwa ulikuwa ni halali, ukeketaji wa mabinti ulikuwa ni halali na mpaka sasa binti analipiwa mahari akibadilishiwa mji wa mwanaume kutoka kwa baba kwenda kwa mume, haina maana ni adilifu. Kuweka sheria zinazohalalisha ubazazi ni sababu tu ya UBINAFSI.
JE,BADO BINADAMU NI MSTAARABU?
Kuwa mstaarabu ndio uongee ustaarabu, acha kuuza binadamu wenzio, ndio uongee ustaarabu, acha kukandamiza wanawake, watoto, maalbino na walemavu wengine ndio uongee kuhusu ustaarabu. Acha kubagua umiliki wa rasilimali kwa kigezo cha rangi na jinsia ndio uongee kuhusu ustaarabu, acha kulipia au kukubali malipo ya mahari na kukeketa wanawake ndio uongee ustaarabu. Linda mazingira , acha kupigania mipaka ya kuchorwa kwenye karatasi ndio uongee kuhusu ustaarabu. Acha kuwagawia watoto makabila na dini, concepts zinazoishi vichwani zikiwagawa kiasi kuchukiana na mwisho, acha kuonea wanyama ndio tuongee kuhusu ustaarabu. Kwa yeyote ambaye ataona picha hizi mbili chini ni tofauti basi hayuko tayari kuanza safari ya kustaarabika. Kwa niaba ya wanyama wote, Nawasilisha!
Mwaka 2010 aliyekuwa Askofu mstaafu wa kanisa la kilutheri Tanzania (ELCT), marehemu Ambilikile Mwasapile alitangaza kuwepo kwa dawa inayotibu magonjwa yote ikiwamo magonjwa sugu kama Kisukari, Kansa na Kifua kikuu dawa ambayo kwa mujibu wa maelezo yake ilitokana na maono ya ndoto aliyooteshwa na Mungu. Mwasapile alituhumu pia dawa hiyo kutibu maambukizi ya virusi wanaosababisha kushuka kwa kinga (Ukimwi).
Babu (kama alivyofahamika na wengi) alitembelewa na watu wa kila rika, na jinsia, viongozi wa serikali, taasisi na vitengo binafsi, masikini na matajiri, na wote walimiminika kuungana na mamilioni ya Watanzania waliokata tamaa kwa kuelemewa na maradhi. Kama haitoshi maelfu wengine kutoka nchi jirani pia walifurika kwenye mji wa Loliondo jijini Arusha ambako ndiko yalikuwako makazi ya Askofu kwa muda huo, kwenda kujipatia dawa hiyo.
Miongoni mwa waliokuwepo kwenye umati huo alikuwamo Mama U (si jina halisi nikikusudia kuficha utambulisho) aliyesafiri kwa zaidi ya kilometa 600 kutoka Dar es salaam kufuata bidhaa hii adhimu ya matumaini. Mama U alikuwa mwathirika wa virusi vinavyosababisha Ukimwi na alikuwa anatumia dawa za kupunguza makali ya virusi hao za ARVs kwa zaidi ya miaka mitano. Aliungana na mamia ya majirani wa mtaani kwake kwenda Loliondo. Alifunga biashara yake ya mgahawa kwa muda, akachukua pesa zake za akiba kwenda kushiriki uponyaji.
Alikaa huko kwa wiki moja na siku kadhaa kusubiri zamu yake kwani umati ulikuwa mkubwa mno. Mamia kwa mamia walikosa dawa na kwa mujibu wa ripoti kadhaa, wagonjwa wengine walifariki kabla hata ya kufika nyumbani kwa Babu. Hali ya miundombinu muhimu kama usafiri, malazi na upatikanaji wa chakula na maji safi haikulingana na idadi ya ghafla ya watu waliofika kwenye mji huo kupata dawa, lakini kwa babhati nzuri Mama U alikuwa miongoni mwa wachache waliofanikiawa kupata dawa na alirudi Dar es salaam kuanza maisha mapya akiwa na tumaini la uponyaji.
MAISHA MAPYA, TUMAINI JIPYA
Mama U alikuwa na nuru usoni, afya mwilini, pia matumaini kichwani kiasi alifanya maamuzi ya kuacha kutumia dawa za kupunguza makali ya virusi wanaosababisha Ukimwi ARVs. Kwa mwezi mzima aliokuwa anaishi bila hizi dawa alikuwa na afya njema tu. Aliwashuhudia watu ukuu wa Mungu wake kwa uponyaji alioupokea. Hakwenda kuthibitisha kupona kwenye kituo cha afya kwa madai kuwa ana imani hana tena maambukizi.
Alitumia muda wake mwingi kutoa ushuhuda wa tiba ya kikombe kwa waliomzunguka na kwa mara ya kwanza maishani mwake alikuwa huru kutangaza rasmi kuwa alikuwa mwathirika kabla yakupoea uponyaji kwani mwanzo alifanya siri. Alikuwa ni chachu ya watu wengine wengi waliomzunguka na waliomsikia kushawishika kwenda Samunge kupata bidhaa. Alikuwa habari ya mji, alialikwa mpaka kwenye mikusanyiko ya kidini tofauti kutoa ushuhuda na kushawishi mamia wengine waliotilia shaka tiba ya Babu. Aliokoka rasmi na kuwa muumini wa kanisa fulani la kilokole na kati ya maagano aliyoyafanya ni kutumia afya aliyojaaliwa kueneza habari njema za Mungu (injili). Yote haya yalitokea ndani ya wiki sita tu tangu apate kikombe cha dawa ya babu.
TUMAINI NI BATILI
Ilimchukuwa Mama U miezi mitatu kuanza kudhoofu mwili kwa sababu ya kuacha kutumia ARVs. Marafiki wa karibu walimshauri kurudia dawa lakini Mama U aliwajibu kuwa anapitia majaribu na hatayumba kwani ana imani kuwa alipokea uponyaji. Alizishuhudia ndoto kadhaa alizoota wiki ya kwanza ya uponyaji zilizomthibitishia kupona. Alizishuhudia kwa kila aliyemtembelea na alizisimulia kwa watu kadhaa waliomshauri kurudia tiba ya hospitalini.
Miongoni mwa nukuu alizokaririwa akisema ilikuwa ni "Mtumishi Ayubu aliuliwa mifugo yake yote, mazao yake yote, watoto wake wote, akapata maradhi lakini aliendelea kumtumaini Bwana" . Aliendelea kukaidi ushauri wa wapendwa waliomzunguka na imani yake ilikuwa imara. Aligombana na rafiki zake wa karibu waliokuwa wanamhudumia anapozidiwa kwa sababu alikataa kunywa dawa.
TUMAINI BATILI LINAFIFIA
Alidhoofu kupita kiasi, mwili uliisha, macho yalipoteza nuru, ngozi iliunda makunyanzi na nywele zilibadilika rangi. Maradhi yaliambatana na kukata tamaa, hofu na hasira (pengine ni kwa sababu alihisi kudanganywa) kwani siku moja alimpiga rafiki yake aliyekwenda kumsaidia usafi nyumbani kwake akimtuhumu kumtangazia habari za kuugua kwake. Aliwapiga watoto wake akihisi wanamsema kwa watu na mtoto wake mmoja alitoroka nyumbani kukimbia kadhia inayoletwa na hali ya mama yake. Mwili wake ulishuka kinga na kuwa jamvi la mwaliko wa magonjwa yote nyemelezi (opportunistic diseases), mara maralia, mara kifua kikuu, mara kuhara.
Alishindwa kufanya kazi yake vyema, hivyo uchumi wake uliingia matatani na hata alipopata nguvu za kupika kwenye mgahawa wake watu waliogopa kwenda kwa sababu mbalimbali kama kinyaa, huruma na wengine walikuwa na imani kuwa upo uwezekano wa wao kupata maambukizi kwa kula chakula cha mwathirika. Washirika wake kibiashara walimkimbia kwani hali yake kiakili haikuwa rafiki wa wateja. Walienda kuendeleza shughuli mahala pengine. Alibaki peke yake, yeye na bidhaa ya tumaini alilouziwa kwa shilingi 500, bidhaa ya mazingaombwe iliyodumu kwa miezi kadhaa tu. Si tu afya yake ya mwili na akili vilikuwa rehani, ndoto zake za maisha, mipango yake na ustawi wa familia yake vyote vilikuwa kwenye ubao mdogo mbovu juu ya bahari iliyochafuka.
Mama U alifariki dunia miezi mitano toka asitishe matumizi ya ARV, kifo kilimkuta akiwa njiani akirudi Loliondo kujaribu kikombe kingine. Aliacha watoto watatu wakiwa bado wadogo sana na rasmi wakawa yatima kwani baba yao alifariki miaka kadhaa kabla yaMama U. Napata picha Mchungaji wa kanisa lake alisema "ni mipango ya Mungu", au "yeye alitoa na yeye ametwaa" na waumini walijibu "jina lake lihimidiwe".
Wakati Mama U akitangulia udongoni, Askofu aliendelea kuuza matumaini kwa waja wengine waliokata tamaa na Serikali ilimpa usaidizi kama kibali cha shughuli, kibali cha tiba na usaidizi kwenye miundombinu ya kiusalama, usafirishaji na huduma muhimu ili kuhakikisha bidhaa hii ya matumaini inawafikiwa na wengi na kwa haraka. Serikali ilithibitisha dawa haina madhara yeyote. Narudia DAWA HAINA MADHARA YEYOTE. Picha iliyokuwamo kwa wahusika serikalini ni KAMA HAIUI UKINYWA BASI NI SALAMA. Matokeo kando ya hii dawa kama hili la mama U halikuwa miongoni mwa shaka kuu la matumizi ya dawa hiyo.
NINI TUNAJIFUNZA?
Kabla ya hadithi ya kweli ya Mama U, Mwaka 2007, Mtanzania Emmanuel Didas alifanyiwa upasuaji wa kichwa badala ya mguu kwa kilichosemwa kuwa ni kuchanganywa kwa taarifa zake na mgonjwa mwingine Emmanuel Mgaya. Kufidia uzembe huu Taasisi inayojihusisha na masuala ya mifupa MOI kwenye hospitali ya muhimbili (waliopolazwa Emmanuel Didas na Mgaya) iliwapeleka wahanga wa tukio hili India kwa matibabu na kwa amri ya mahakama walikubali kulipa kiasi cha shilingi milioni 100 kwa Didas aliyewashitaki MOI kwa madai (compesation for the injuries). Ripoti kadhaa zinasema uongozi wa Muhimbili uliwashughulikia wahusika kwa uzembe, sina shaka walisimamishwa kazi kwa muda au labda moja kwa moja au hata serikali kuwafutia leseni za udaktari.
Madaktari wana nguvu kubwa ya kuaminisha umma juu ya usalama na ufanisi wa dawa au taratibu za kimatibabu (medical procedures). Mara nyingi mtu yeyote mwenye haja ya tiba anachukua maoni ya kitabibu kutoka kwa daktari as literal and correct information. Haya mamlaka waliyonayo madaktari wanayo pia watabibu kando kama wachungaji, waganga wa jadi na wataalamu wa tiba za nyumbani (HOMEOPATHY) au hata wasoma nyota. Lakini linapokuja suala la kuwa accountable for malpractices Wachungaji wanaotuhumu kuponya hawaguswi. Mama U alikuwa ni alama moja tu kuwakilisha wengi waliofariki kwa kuacha matibabu rasmi ya kitaalamu yaliyothibitishwa kitaalamu.
National library of Medicine (NIH) wanaeleza kuwa makosa ya kidaktari (medical malpractice) ni kosa kisheria na ni kipengele mojawapo cha TORT. Labda kifo cha Mama U siTORT kama tu yalivyo makosa yeyote ya kimatibabuyanayoweza kufunguliwa kesi za madai kama hiyo ya Emmanuel Didas. Je nani atawazungumzia waathirika wa madaktari wa tiba kando/mbadala na wafanyabiashara wa kuuza matumaini na kuwaomba kuthibitisha matumizi ya bidhaa zao kabla ya kuwapa watu? Na inahitajika watu wangapi kufariki kwa imani hizi ili iwe ni miongoni mwa mada kuu za mazungumzo kwa jamii na serikali na kuacha kuwa faragha?
Kuna haja gani ya wataalamu kuthibitisha dawa kama zimefikia kiwango cha ubora ambao serikali imejiwekea ikiwa wapo waganga wa jadi, wataalamu wa tiba za majumbani (HOMEOPATHY) na wachungaji wanaotoa hizi tiba bila kibali cha ubora na usalama kwa gharama za pesa, muda na maisha ya watu?