Msanii wa muziki kutoka nchini Tanzania, Dizasta Vina ni mmoja wa viongozi katika orodha ya wafalme wa Hip-Hop wa kizazi cha leo. Muziki wake umebeba falsafa, mafunzo na mitazamo inayogusa jamii kwa namna tofauti. Ana mtindo wa kipekee, mashairi yenye ujumbe na mtiririko wa visa na matukio ya maisha halisi ya kila siku.
Mwanzoni mwa mwaka 2021, Dizasta alitoa albamu ya "The verteller". Ni albamu yake ya pili, ina vibao 20 vinavyo ongelea tamaduni, mitazamo na imani ya vikundi mbalimbali vya watu wa jamii aliyotokea. Albamu inatoa picha ya maisha ya watu wa jamii yake, misimamo yao dhidi ya msimamo wake kuhusu masuala mbalimbali na hadithi nyingine zinazogusa nyanja mbalimbali za maisha ya binadamu.
Kabla hujaamua kwenda kununua albamu hii au kuisikiliza kwa mara nyingine fuatilia simulizi ya Dizasta Vina kuhusu safari ya kuandaa albamu ya The Verteller, hadithi za kuvutia za baadhi ya nyimbo zake, na maelezo ya kina ya ubunifu wake.
Kuhusu jina la "The Verteller".
“ Niliipa albamu jina la The Verteller kwa sababu za kisanaa na kibiashara. Jina linasikika na kuandikika kisanaa kuliko tafsiri yake kwa lugha nyingine ikiwemo lugha mama ya mwandishi, lugha ya Kiswahili. Neno 'verteller' lina maana ya ‘msimuliaji’ kutokea lugha ya Kidachi, the storyteller au rawi kwa kiingereza na kiarabu na majina mengine kwa lugha tofauti hayakuwa na mwonekano uliovutia kimaana na kiumbo kutumika kama jina la albamu kuliko 'The Verteller' na pia kwa sababu za kibiashara lilikuwa ni neno jipya kutumika kwenye kiwanda chochote cha burudani hasa kama albamu ya muziki".
Albamu inaitwa The Verteller kuwakilisha wasifu wa msimuliaji na mahala anakotoka. Jina hili linasanifu maudhui kwani albamu imesheheni masimulizi ya matukio yanayotokea mahala anapotokea msimuliaji kwa maana ya mtaa, mkoa au nchi. Dizasta Vina anasema “The verteller inaonyesha taswira ya elimu, imani, tamaduni na mila za jamii yangu na jinsi zilivyojenga mtazamo wangu wa sasa”.
Muda uliotumika kuandaa albamu.
The Verteller ilikuwa kwenye maandalizi kwa muda mrefu. Nilitumia muda mrefu kuiandaa na moja ya sababu ni kwamba kulikuwa na wazo la pili kwenye kila hatua. Mfano mmoja kwenye uchaguaji wa midundo, nyimbo nyingi zilizokuwa zimerekodiwa na midundo tofauti na ile inayosikika kwenye albamu. Muziki ulibadilishwa kila wazo jipya lilipokuja, yote ikilenga kuwa na muziki mzuri unaoendana na maudhui, hali na msisimko wa nyimbo husika. Albamu ilichukua karibia miezi 26, kuanzia kuandikwa hadi kuzalishwa na kusambazwa sokoni.
Wimbo unaomuhusu yeye binafsi.
“Kuna nyimbo nyingi ambazo zinanihusu mimi, karibu zote japo sio kama hadithi zinavyosema lakini falsafa nyuma ya hadithi au mitazamo ninayowakilisha. Kuna nyimbo zinanihusu moja kwa moja, mfano 'Yule Yule' - Yule yule nimezungumzia mahara nilipotoka, jinsi nilivyoishi, watu na itikadi zao, jinsi wanavyo ishi huko, na jinsi wanavyoona jamii ya watu wengine. Nyimbo nyingine zote ni simulizi za kubuni lakini zinaendana na hadithi ambazo nimezitoa mtaani kwangu”.
The verteller ni wasifu wa maisha ya mwandishi ambaye ni mimi. Naonyesha nilipotoka kukoje, kwa mfano hadithi za “Kibabu na binti” zipo kwenye mitaa niliyotoka, “Tattoo ya asili” zipo kwenye mitaa niliyotoka, “Confession of a mad man” ambayo inaonyesha jamaa anakutana na binti anamwambia binti ondoka, usipoondoka nitakufanyia hiki na kile binti anahisi anamtania, ni sitiari ya watu wanaotoka kijijini na kuingia mjini kwa mara ya kwanza. Kuna kuwa na kila dalili mbaya ya kupata shida akija mjini lakini anapuuzia dalili hizo kwa matumaini kwamba labda siku moja mambo yatakuwa bora zaidi. Zote hizi zina wakilisha baadhi ya maadili na falsafa ninazoziamini, kwahiyo zinanihusu kwa njia moja au nyingine.
Utofauti wa albamu ya ‘The Verteller’.
Utofauti wa albamu ya “The Verteller” na album nyingine nyingi za Hip Hop hapa Tanzania ni kwamba ni wasifu wa msimuliaji na mahala alipotoka (Biography). Msimuliaji anaeleza jinsi mwanamke anavyoonekana, na nafasi yake katika jamii, masuala ya mahusiano jinsia na watoto, uhuru wa kuongea na vyombo vya habari, ukimwi na watoto wa mitaani, usalama na mtoto anavyoonekana kwenye jamii yake na vile anavyolelewa. Msimuliaji anaeleza hivyo vitu vilivyo athiri namna anafikiria na vile anavyoishi. Ni miongoni mwa albamu chache ambazo zimefanywa hivyo.
Kwa mtazamo wa kisanaa ni albamu ambayo asilimia 90 ya nyimbo ni hadithi ambazo visa vyake zimebuniwa lakini zinaelezea mambo yanayohusiana na sehemu msimuliaji ametoka. Ni albamu ya simulizi, kitu ambacho hakijawahi kutokea Tanzania lakini pia ni wasifu wa msimuliaji, inaonyesha msimuliaji tangu anaanza alipozaliwa mpaka hapa alipo, kule alikotoka na jinsi jamii ilivyomlea, mabaya na mazuri aliyoyaona kwenye jamii yake ndio anakuja kuyasimulia.
Wimbo uliochukua muda mrefu kuuandaa.
Kuna nyimbo kadhaa zilichukua muda mrefu, Hatia namba nne ni mojawapo kwa sababu ilibadilishwa kutoka kwenye riwaya kuwa wimbo. Anasema “ilitakiwa nipunguze baadhi ya vitu nijue kitu gani ni muhimu sana kukiweka kwenye wimbo, kitu gani nikitoa kitaharibu maana na mtiririko wa sehemu za wimbo au wimbo mzima”.
Ilichukua muda mrefu kurekebisha kwa sababu kulikuwa na mabadiliko mengi - inatakiwa utengeneze wimbo, utengeneze namna utawakaribisha wasikilizaji kwenye wimbo, uwashawishi wabakie halafu uwapeleke kwenye uelekeo mmoja baadae ubadilishe ule uelekeo haraka kuleta mvuto kwenye hadithi. Ili kuwa ni kazi ngumu kuiandaa, hata Ringle Beats ilimchukua muda mrefu kwa sababu tulijaribu midundo mingi na kubadilisha maana mingine ilikuwa inaharibu hisia za wimbo, mwisho wa siku tulipata mdundo sahihi, tukaufanyia kazi na watu wakaupenda.
Kuhusu kutayarisha muziki na Ringle Beats.
Mimi na Ringle Beats tumekuwa marafiki kwa miaka mingi sana, tumefahamiana mwanzoni mwa mwaka 2011 ni kama miaka 10 sasa na tumekuwa marafiki tangu hapo. Alitayarisha nyimbo ya kwanza ya Panorama ya mimi na Dubo na kutoka hapo tumekuwa karibu. Ametayarisha nyimbo zangu nyingi, Kanisa, Siku mbaya, NIS3, Waite hakika tumekuwa marafiki kwa muda mrefu. Alikuwa mtu wa kwanza kumfikiria lilipofikia wazo la kusema nifanye na mtayarishaji gani.
Ringle Beats alikuwa mtu wa kwanza kumfikiria kwa sababu tunafahamiana muda mrefu na nafahamu uwezo wake wa kutayarisha kazi, pia ana historia ya kufanya shughuli za muziki kanisani kwenye kwaya, ana utaalam na mbinu nyingi za kutayarisha na kuchanganya muziki. Ni mhandisi mzuri wa sauti, pia ni mbunifu anapiga kinanda vizuri, gitaa na ala nyingine za muziki, ana uwezo mkubwa kwenye kutayarisha muziki. Tumefanya na watayarishaji wengine kadhaa ambao walikuja kuchangia utaalam na maoni yao. Cjamoker na Jcob walichangia "mixing na mastering" na kuna watayarishaji wengine lakini mtayarishaji mkuu ni Ringle Beats. Kwenye kuandaa muziki uwezo wake unagusa sehemu kubwa ya utayarishaji hii ilikuwa ni faida sana kwangu.
Wimbo maalum zaidi.
Nadhani albamu nzima ni maalum kwangu, lakini kuna nyimbo ambazo naona kwangu ni maalum zaidi. Hatia namba nne ni maalum sana kwangu kwa sababu nilitaka kuandika kitabu lakini nikaona inafaa sana kuwa wimbo, nilirekebisha vitu vingi ili kitabu kiwe wimbo, utayarishaji wake ulisumbua kubadilisha mawazo kutoka kwenye kitabu kuwa wimbo, hakika kila wakati nikisikiliza huu wimbo najisikia fahari sana kwa jinsi ulivyotoka.
Lakini Mwanajua ina maana binafsi kwangu, maana ambayo nimeacha watu waitafute. Kuna watu ambao tayari wanajua maana ya Mwanajua kwa sababu wameelewa fumbo nililoliweka kwenye wimbo. Watu wengine wametengeneza maana zao jambo ambalo ni sahihi kwa sababu sijawahi kuiweka hadharani kila mtu akaelewa maana yake, kuna watu wanaohisi ni binti mrembo, wengine wanahisi ni umaarufu ambao unakuja na kuondoka, vyeo, maisha yanakuja na kuondoka wote wapo sahihi nilichotaka ni wimbo kugusa watu, kama wimbo umekugusa na umetengeneza maana yako binafsi ni sawa, kwa hiyo mwanajua ni maalum kwangu, yule yule ni maalum zaidi kwangu kwa sababu unahusu msimuliaji mwenyewe.
Ujumbe uliojificha kwenye mpangilio wa nyimbo.
Mpangilio wa jumla wa albamu ni kwamba msimuliaji anazaliwa, msimuliaji anajifunza na kisha anafanya makosa, anaingia kwenye mapenzi, anajuta, msimuliaji anapata faraja na mwisho wa siku msimuliaji anakufa. Maudhui kadhaa ya mwanzo yanaonyesha kuanza yani mwanzo, maudhui yanayofuata yanaonyesha kukua, maudhui ya katikati yanaonyesha makosa na maudhui ya mwisho yanaonyesha msimuliaji anakufa. Mpangilio wa jumla hakuna nyimbo maalum zinazoeleza kuzaliwa na kufa lakini maudhui yaliyopo kwenye maeneo ya mwanzo, katikati na mwisho yanaonyesha yupo kwenye kuzaliwa, kukua, kufanya makosa, kutubu na kisha kufa.
Msukumo katika kuandaa albamu.
Dizasta anasema “nilisikiliza sana albamu ya ‘Mi Mmasai’ ya Mr Ebo na ‘Machozi, jasho na damu’ ya Professor Jay wakati naandaa albamu hii kwa sababu hizi albamu zilikuwa na maudhui mengi sana. Nilikuwa nafuata msukumo chanya humu, lakini nilikuwa nanoa ufundi wa kutiririka kutoka kwenye sanaa nyingine tofauti ila katika kuandaa The Verteller nilipata msukumo zaidi kwenye hizi kazi mbili”.
Maudhui ya albamu.
Dhamira kuu ya albamu ni uhuru wa kuzungumza na kujieleza ndio maana utangulizi unasema msimuliaji aachwe huru ili waovu watangazwe na wema washangiliwe. Kuna dhamira nyingine ndogo ndogo nje ya wazo kuu nazo ni kama ifuatavyo.
Dizasta Vina anamzungumzia mwanamke anavyoonekana kwenye jamii yake ambapo wengi wanamtumia kama chombo cha starehe, wengine wanaona kama hana sauti hivyo mawazo yake hayaheshimiki kwenye jamii ambayo msimuliaji katoka (binti anabakwa kwenye wimbo wa tatuu ya asili). Kwenye albamu hii mwanamke pia anazungumziwa kama kiongozi kwenye jamii yake, wimbo wa "A confession of a mad son" na sehemu kadhaa za wimbo wa "Yule yule" msimuliaji anaeleza alivyolelewa na mama yake, hii inaonyesha nafasi ya mwanamke kama kiongozi.
Msimuliaji pia anazumgumzia masuala ya jinsia na nafasi za kila jinsia kwenye jamii, wimbo wa "Mascular feminist" na sehemu baadhi za "Wimbo usio bora" zinazungumzia nafasi ya kila jinsia kwenye jamii.
Masuala ya maadili yamezungumziwa kwenye nyimbo kama "Wimbo usio bora" na “Mlemavu” ambapo mume ana mlalamikia mwanamke kubadilika na kukosa maadili, pia kwenye "Tatuu ya asili" vijana walimbaka binti kwa kukosa malezi mazuri yaliyopelekea kuwepo kwa mmomonyoko wa maadili.
Kwenye nyimbo kama "Ndoano" na “wimbo usio bora” amezungumzia mapenzi, mahusiano na ndoa, nyimbo nyingine zilizogusa masuala ya mapenzi ni pamoja na “Mlemavu”.
Pia kwenye wimbo wa "A confession of a mad philosopher" na wimbo wa "Kifo" msimuliaji amezungumzia falsafa nyuma ya pumbazo la uhuru wa nafsi na hiari ya kufanya maamuzi (Free will illusion).
Dhamira nyingine ndogo ndogo zilizoonekana kwenye huu mradi ni kama uhuru wa vyombo vya habari, watoto wa mtaani, ukimwi, umuhimu wa elimu kwa jamii na matumizi mabaya ya madaraka, wimbo wa "Tattoo ya asili" mwalimu alikatazwa kuongea na kiongozi, alitumia nafasi yake kukandamiza maoni ya watu wengine na pia alizongwa na ujinga. Dizasta Vina anasema "Sehemu ambayo elimu itadharauliwa na kuwekwa chini ndio sehemu ambayo matatizo yataibuka" kwa hiyo kuna umuhimu wa elimu kwa jamii.
Dizasta amejadili madhara ya mihadarati, kamali na Rushwa kwenye wimbo wa “Money”, ukimwi na tabia chochezi kwenye kuenea kwenye “tatuu ya asili” na athari za kuwepo kwa watoto wa mitaani.
Kuna mgogoro kati ya kundi na kundi au mtu na mtu. Mfano, wanandoa wana kwazana kwenye “Wimbo usio bora”, kiongozi na wananchi kwenye “Tatuu ya asili”, askari na raia kwenye “Money” na baba na mtoto kwenye “Kibabu na binti”.
Pia kuna migogoro nafsi au dhahania. Mfano, mwandishi anaongea na kifo nafsini kwenye wimbo wa “Kifo”, anawaza kuhusu uhuru wa nafsi kwenye “Confession of a mad philosopher”, mwanamke na mwanaume “muscular feminist”, pia mwandishi anawaza jinsi Mwanajua alivyoondoka baada ya kutamba sana “Mwanajua”.
Mwandishi amejadili matatizo ya afya ya akili alipojadili ugonjwa unaoitwa “ASPERGERS” ambayo ni hali inayosababisha kukosa uwezo mzuri wa kuchangamana na jamii na kuwasiliana. Kwenye wimbo wa “Yule yule” Dizasta alikili kuwa na hali hiyo.
Dizasta anatupa jumbe kadhaa. Mfano, anasema umaarufu, pesa na vyeo vinapita kwenye “Mwanajua” na “Almasi”, elimu ni ukombozi kwenye “Tatuu ya asili”, tamaa inaponza kwenye “Money”, ndoa si mafanikio kwenye “Ndoano”, usawa ni fursa si matokeo kwenye “Muscular feminist” na uhuru si kitu halisi “Confession of mad philosopher ”.
Nunua albamu hii au isikilize kwenye Audiomack, Boomplay na mitandao mingine na tufahamishe nyimbo unazozipenda kwenye albamu kupitia kurasa za Panorama Authentik kwenye Facebook, Instagram na Twitter.